Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiwapungia wanaCCM waliofika kwenye Ofisi ya CCM ya kata ya Kibaoni kumdhamini katika nia yake ya kuwania uteuzi wa CCM katika kugombea nafasi ya urais Juni 15, 2015.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akisalimian na baadhi ya wananchi wa Mpanda waliofika kwenye ofisi ya CCM ya Wilaya ya Mpanda kushuhudia na kumdhamini ilia pate sifa za kuteuliwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Juni 15, 2015.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akisalimiana na baadhi ya wanaCCM wa kijijini kwake Kibaoni wilayani Mlele Juni 15, 2015 wakati alipokwenda kwenye Ofisi ya CCM ya kata ya Kibaoni kabla ya kudhaminiwa na wana CCM wa kata hiyo katika nia yake ya kutafuta uteuzi wa CCM wa kugombea urais katika uchaguzi uja.
Baadhi ya wananchi wa Mpanda waliofika kwenye ofisi ya CCM ya wilaya ya Mpanda kumdhamini Waziri Mkuu, Mizengo Pinda katika nia yake ya kuwania uteuzi wa CCM kugombea nafasi ya rais wa Tanzania Juni 15, 2015.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ambaye pia ametangaza nia ya kuwania urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) amepata wadhamini 9,141 baada ya kuhitimisha zoezi hilo katika mkoa wa Katavi.
Hadi jana mchana alikuwa amekwishapata wadhamini 4,243 kwa kuzuru vituo viwili tu vya Inyonga na Mpanda Mjini. Lakini hali ilibadilika alipofika kijijini kwao Kibaoni kwenye ofisi CCM kata ya Kibaoni ambako alikuta maelfu ya watu wakimsubiri ili wasaini fomu za kumdhamini.
Akitangaza idadi ya watu walijitokeza kumdhamini Waziri Mkuu, Katibu wa CCM wilaya ya Mlele, Bw. Sidael Goroi alisema kuwa tarafa za Mpimbwe na Mamba ambazo ziko kwenye Bonde la Ziwa Rukwa zimetoa wadhamini 3,450 wakati tarafa ya Nsimbo imetoa wadhamini 1,448 na kufanya jumla ya wadhamini 4,898 kwa jana jioni tu. Tarafa ya Mpimbwe ambako Waziri Mkuu anatoka ina kata tisa zikiwemo za Kibaoni, Mwamapuli, Ikuba, Usevya, Mbede na Majimoto.
Mapema jana asubuhi, katika kituo chake cha kwanza cha Inyonga, yalipo makao makuu ya wilaya yake ya Mlele, Waziri Mkuu alipata wadhamini 1,440. Alirejea Mpanda saa 9 mchana ambako katika ofisi ya CCM Wilaya alipata wadhamini 2,803 na kufanya jumla ya wadhamini 4,243 kwa vituo hivyo viwili.
Akitoa nasaha zake kwa wakazi hao jana jioni (Jumatatu, Juni 15, 2015), Waziri Mkuu aliwashukuru wote waliomdhamini huku akiwaomba waendelee kumuombea safari zote zilizo mbele yake na zoezi zima liende vizuri kwani suala la urais siyo lelemama bali ni la kumtanguliza Mungu.
Akifafanua zaidi, Waziri Mkuu Pinda alisema: “Suala la urais si la kufa na kupona bali ni la kumtanguliza Mwenyezi Mungu kwanza. Kila mgombea anapaswa amuombe Mungu kwamba kama itampendezea na kumuona anafaa ndipo amchague yeye (mtangaza nia).”
“Ndiyo maana mara zote huwa nawaambia wenzangu kwamba hakuna haja ya kutukanana wala kupakana matope. Huwa nawaambia tusikwaruzane wala tusitukanane kwa sababu hakuna ajuaye Mwenyezi Mungu amemuandaa nani miongoni mwetu,” alisema.
Aliwataka wananchi na viongozi wa wilaya hiyo watoe ushirikiano kwa wagombea wengine watakaofika wilayani humo kuomba wadhamini.
No comments:
Post a Comment