Sunday, December 1, 2019

DKT MUHAMMED SEIF KHATIB MTUNUKIWA WA KWANZA WA PhD CHUO KIKUU DODOMA

Na  Mwandishi wetu

Alipohojiwa mnamo January mwaka juzi, Dkt. Muhammed Seif  Khatib alikuwa na mengi ya kuzungumzia kuhusu umuhimu wa kuhifadhi historia, ambapo aliweka bayana kwamba wakati umefika wa kujenga makumbusho ya Taifa ya Mapinduzi ya Zanzibar, ili kizazi cha sasa na kijacho kiweze kujifunza na kuipitia historia muhimu kwa Watanzania na wageni kutoka nje.

Dkt. Khatib anasema ni vema kuonesha  katika  picha,  filamu,  maandishi  na  sura  halisi  za  historia  ya  Zanzibar ya wakati huo uliopita wa utawala wa wageni wa Waajemi, Wareno, Waarabu, Waingereza na hadi hivi sasa wakati wa Serikali ya Mapinduzi ya Waafrika inaongozwa na walio wengi. 

“Kwa kuweka makumbusho na usahihi wa historia ya nyuma ya kabla, wakati na baada ya Mapinduzi kadhalika na yanayotokea hivi sasa, hayo yote yakiwa katika makumbusho hio, yatakuwa msingi wa historia ya Zanzibar hatua ambayo itasaidia kuwekwa wazi mambo yaliyowahi kutokea, hivyo sio rahisi kwa mtu yoyote ambaye ana agenda ya kupotosha umma kufanya hivyo”,  alisema Dkt. Khatib ambaye unapokutana naye bado anaonekana ni mwenye nguvu zake na afya tele.

Ila kwa vile wazo lake la kuwa na kituo cha historia halijafanyiwa kazi, bado Dkt. Khatib tu anasikitika kwamba hivi sasa ni kweli kabisa mtu yoyote anaweza akasema vyovyote atakavyo kwa kuwa haijui historia vema na wala hana mahali pa kurejea historia ya Mapinduzi ya Zanzibar.  

“Wengi hawajui kwamba watu walitoka Kongo, Malawi, Kigoma na Tabora wakibebeshwa pembe za Ndovu na kusafiri kwa mguu, wakifuata njia ya reli ya kati, mpaka Bagamoyo na kusafirishwa na  jahazi  mpaka  Unguja  na  kuwekwa  sokoni  kuuzwa  kama  samaki  katika  soko  la watumwa. Huu ndio ukweli ambao sio tu wengi hawaujui, bali pia yapasa waujue” anasema Dkt. Khatib.

Anatoa  mfano  wa Rwanda  iliyokumbwa na  mauaji  ya  kimbari  mwaka  1994,  na kwamba kwa kutambua kuwa hicho siyo kitu kizuri kutokea tena hapa duniani nchi hiyo imeweka makumbusho ya kitaifa ambayo japo yanahuzunisha lakini ndio ukweli wenyewe. 

“Ukweli kwenye makumbusho hayo mjini Kigali utajionea maelfu ya mafuvu ya vichwa vya watu waliouwawa yalivyopangwa kiasi hata huwezi kuamini kama hiyo ndiyo iliyokuwa hali halisi ya mauaji ya kimbari yalivyotokea hapa duniani.

“Kwa Wanyarwanda na watu wengine duniani, makumbusho ya kimbari ni sehemu ya Utalii ikizingatia msemo wa waswahili wanasema kuona ni kuamini”, anasema Dkt. Khatib. 

Anaongeza kwamba siyo Rwanda tu, bali hata nchi ya Namibia kuna jumba la makumbusho la mauaji yaliyofanywa na Wajerumani kwa kabila la Waherero ambao anasema waliuwawa katika vita ya kwanza ya dunia, ambapo takribani Waherero nusu ya milioni waliuwawa na hivi karibuni Waherero wa Namibia walikuwa wanaomba fidia kwa Serikali ya Ujerumani, ingawa Ujerumani wameomba msamaha kwa mauaji hayo ya kimbari.

Dkt. Khatib anasema kwamba Uingereza ni nchi inayoongoza duniani kwa kuweka kumbukumbu zake katika makumbusho za kifalme, Kimataifa, Kitaifa, Vita, Silaha, Bahari, Mtu Binafsi, Jiji au Mji husika, ikiwa ina zaidi ya makumbusho 55 ambayo yanafahamika duniani. Mfano ikiwa ni British Museum London, Natural History Museum London, National Gallery London, Science Museum London, Victoria ana Albert Museum, National Maritime Museum, Museum of London City, National Portrait Gallery, National Army Museum, Sir Johns Soanes Museum, Wallace Collection London, National War Museum na kadhalika.

“Kujengwa kwa kituo cha makumbusho Zanzibar pia kitasaidia kuingiza fedha ikiwa kama sehemu ya Utalii wa historia kama wanavyofanya nchi zingine, ambapo mtu anayehitaji kuijua historia hiyo atapata kila kitu mahala pamoja bila kusumbuka”, anamalizia Dkt. Khatib.

Yote hayo tisa, mimi baada ya kufanya utafiti wa kina nikakuta kumbe hata yeye mwenyewe Dkt. Muhammed Seif Khatib ni mmoja wa watu ambao watafaa kuandikwa historia zao na kuwemo kwenye kituo hicho cha kumbukumbu, maana kwa kweli kapita kwingi na kufanya mengi na kuishi kwingi na kuona mengi.

Na endapo mtu akipata kibarua cha kuandika hiyo historia yake yeye kama yeye, hakika utapata taabu uanzie wapi ama fani ipi kati ya nyingi alizopitia na ambazo anazo hadi hii leo - kama ambavyo mimi nimepata shida kuandika hii sehemu tu ya historia yake hapa.

Baada ya kuongea nae kwa kina, nikawa najiuliza sijui nianze na hili jina la Daktari ambalo alilipata rasmi mnamo Novemba 25, 2011 pale alipotunukiwa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Dodoma na Mkuu wa Chuo hicho, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa.

“Hii ilikuwa Shahada ya Kwanza ya PhD kutoka katika Chuo Kikuu cha Dodoma. Ni bahati ilioje mimi kuipata Shahada hii ya juu kitaaluma” anasema Dkt. Khatib huku akiikumbuka vyema siku hiyo katika viwanja vya UDOM, wakati aliposimamishwa na kwenda kupiga goti na mbele ya Mhe. Mkapa na kutunukiwa Shahada hiyo.

Anasema Mada yake ya kuupata udaktari huo wa Falsafa ilikuwa ni ulinganisho wa washairi Shaaban Robert wa Tanga (wa karne ya 20) na Muyaka bin Haji wa Mombasa (wa karne ya 19), akichambua jinsi wanavyomsawiri mwanamke kwa “chanjo za matakwa ya mwanamume”. 

“Nilifarijika kufikia kiwango hicho cha elimu na kutunukiwa na Rais Mkapa ambaye niliyefanya kazi nae kwa muda wa miaka 10, akiamini kuwa mmoja wa mawaziri wake aliowaita “Askari wa Miamvuli”, anasema huku akitabasamu. 

Nikajiuliza labda nianze na historia yake ki-elimu, baada ya kuniambie yeye alisoma hadi darasa la nane lakini alijiendeleza mwenyewe na hatimaye kupata Shahada yake ya Kwanza,  katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1978 na Shahada ya Pili aliipata mwaka 1982 Uingereza SOAS. 

Kwa kweli Dkt. Khatib, ambaye baada ya kuhudumu kupitia Umoja wa Vijana kama mbunge wa viti maalumu baadaye akahudumu kama mbunge wa Uzini kwa miongo kadhaa, ni changamoto kubwa kumwelezea. 

Hasa ikizingatiwa kwamba yeye pia Mwenyekiti wa BARAZA LA KISWAHILI LA ZANZIBAR (BAKIZA), Mwenyekiti wa Mapitio ya Kamusi Fasaha la BAKITA lilochapwa 2010, huku akiwa Mhadhiri wa Muda kwa wanafunzi wa Shahada ya Uzamili (Masters) katika Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA). 

Na kama hayo yote hayatoshi, hivi karibuni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohamed Shein alimteua kuwa Mjumbe wa TUME ya UTUMISHI WA UMMA katika Ofisi ya Rais, Zanzibar. 

Tukija alikokopita huko nyuma, utakuta Dkt. Khatib amewahi kushika nyadhifa nyingi na kwa muda mrefu ikiwa ni pamoja na  kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (1978-82), Katibu Mkuu Umoja huo (1982 - 88) ambapo hapo kwa vijana amekuwa kiongozi kwa miaka 10. 

Amekuwa Waziri katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika awamu ya Pili ya Rais Ali Hassan Mwinyi, na awamu ya Tatu ya Mhe. Mkapa na ya nne ya Dkt. Jakaya Kikwete (1988-2010), safari hiyo akianzia toka akiwa mbunge wa viti vya Vijana na baadaye wa Jimbo la Uzini tokea mwaka 1988 hadi alipostaafu mwaka 2015. 

Vile vile amekuwa Mjumbe wa NEC ya CCM tokea 1978 hadi 2017, Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho (1995-2017), na baadaye Katibu wake wa  Oganaizesheni 2012-2017. 

Licha ya kuwa mwanasiasa mwenye nyadhifa mbalimbali, Dkt. Khatib katika muda wake wa ziada alikuwa mwandishi wa makala za michezo katika gazeti la Serikali la Daily News, gazeti la chama Uhuru na katika Mzalendo akiwika na makala yake mashuhuri KIPANGA. 

Na hakuishia magazetini pekee. Huyu bwana pia ni Mwandishi mashuhuri wa vitabu vikiwemo “Fungate ya Uhuru”, “Wasakatonge”, “Chanjo”, “Vifaru Weusi”, Utenzi wa Ukombozi wa Zanzibar” na “Taarab Zanzibar”. 

Nilipoongea nae hivi karibuni, Dkt. Khatib amenambia kwamba amehamasika sana na kitendo cha Mhe. Mkapa kutoa kitabu cha historia ya maisha yake, na kuongezea yeye pia tayari yuko mbioni kufuata nyayo za kiongozi huyo mahiri kwa kuandaa kitabu cha maisha yake. 

Hapana shaka kwamba kitabu chake hicho kitatuhadithia sio tu alivyokiuwa na kipawa cha kufanya mambo mengi kwa wakati  mmoja, bali pia jinsi alivyokuwa mwanasoka hodari wa timu ya Kikwajuni almaarufu kama “KISK” na timu ya Taifa ya Zanzibar - bila kusahau alikuwa pia Nahodha wa timu ya soka ya Chuo cha Nkrumah. 

Dkt. Khatibu, ambaye anasema hobby zake kubwa ni kufanya jogging, kusoma vitabu na makala mbaklimbali, pia ameshatunga nyimbo kibao za taarabu zinazoimbwa na wasanii wa bendi mbalimbali ikiwemo Culture.  Baadhi yake ni "Nia yangu sigeuzi", "Paka shume", "Wewe peke yako," "Nakupenda" na nyingine kibao.

Hadi nafikia hapa, bado sijajua nianzie wapi kumwelezea huyu mwanasiasa, mwanamichezo, mwanahabari, mshairi, ambaye kwa sasa  anasimamia kwa karibu kampuni ya familia ya Zanzibar Media Corporation akiwa Mkurugenzi wa Zenj Fm na Zenj Tv. 

Mie nashauri tusubiri tu hicho kitabu cha maisha yake ili tumjue kwa undani, na vile vile mamlaka zinazohusika, zikipendezwa, zianzishe hicho kituo cha kumbukumbu na historia ya Zanzibar kama anavyoshauiri - na kujumuisha kitabu chake kuwa miongoni mwa vitu vitavyowekwa humo.  Ama hakika, kwa maoni yangu, anastahili kuwemo kama ambavyo Wazanzibari wengi wa aina yake wanavyostahili.

 Dkt Muhammed Seif  Khatib aliposimamishwa ili kwenda kupiga goti Novemba 25, 2011 pale alipotunukiwa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Dodoma na Mkuu wa Chuo hicho, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa. Hii ilikuwa Shahada ya Kwanza ya PhD ya Chuo Kikuu cha Dodoma toka kianzishwe. 
 Dkt Muhammed Seif  Khatib  alipotunukiwa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Dodoma na Mkuu wa Chuo hicho, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa, Novemba 25, 2011. Hii ilikuwa Shahada ya Kwanza ya PhD ya Chuo Kikuu cha Dodoma toka kianzishwe.
 Dkt Muhammed Seif  Khatib katika tafrija ya kifamilia baada ya kutunukiwa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Dodoma na Mkuu wa Chuo hicho, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa, Novemba 25, 2011. Hii ilikuwa Shahada ya Kwanza ya PhD ya Chuo Kikuu cha Dodoma toka kianzishwe.
 Dkt Muhammed Seif  Khatib (namba 2) akiwa  na kikosi cha "Kiski" miaka ya 1970 
Akiwa Nahodha wa timu ya Chuo cha Nkrumah Dkt. Khatib akipokea kikombe cha ubingwa toka kwa Raisw wa kwanza wa Zanzaibar Sheikh Abeid Amnani Karume

 Dkt. Khatib akimkabidhi Mwalimu Nyerere Tunzo ya Kimataifa akiwa Katibu Mkuu wa Vijana mbele ya Rais Ali Hassan Mwinyi. Anasema hakumbuki mwaka ila kabla ya 1988

Dkt Muhammed Seif  Khatib wa pili kushoto waliosimama mbele. Hili lilikuwa baraza la mawaziri la kipindi cha pili cha Rais wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa. 
Dkt Muhammed Seif  Khatib akiwa katika majukumu yake kama Mkurugenzi wa Zanzibar Media Corporation Ltd., siku kilipoingia makubaliano ya kurusha vipindi vya CCTV ya China



Dkt Muhammed Seif  Khatib akiwa katika majukumu yake kama Mkurugenzi wa Zanzibar Media Corporation Ltd., akiwa na wageni waliotembelea Zenj FM/Zenj TV kutoka Amana Bank baadfa ya kufungua Tawi lao Zanzibar. Kutoka kulia ni Nassor Ameir, Dr.Muhammed Seif Khatib,Farsy Mussa na Jamal .I.Jamal
Ni Mwaka 2005  wakati Marehemu Ali Juma Shamuhuna alipokuwa mgeni wa Heshima katika ufunguzi wa Zenj FM.  Watatu kushoto ni Meneja wa  Zenj FM, Dkt. Khatib (kushoto), mwakilishi wa Mikunguni Mhe. SulShihata na Bwana Subash Patel.


Mwaka 1973 wakati Rais wa Zanzaibar wakati huo Mhe. Aboud Jumbe alipokutana na wajumbe wa Kamati ya kukusanya, kunakili na kuandika kitabu cha hotuba za Rais wa Kwanza wa Zanzibar Sheim Abeid Amani Karume. Dkt. Khatib ni wa tatu kutoka kushoto.
Dkt Khatib akiwa ofisini kwake na Omar Mkambara mtangazaji mahiri wa Soka kutoa BBC aliyekuwa katika maandalizi ya kutangaza mashindano ya AFCON  ' live' kutoka Misri na kupiga kambi Zenj FM  kuwashirikisha Wazanzibari.
Picha ya pamoja ya viongozi wa BAKITA na BAKIZA baada ya kikao cha mashauriano. Kutoka kulia waliosimama mbele ni Bi Mwanahija (Katibu Mtendaji - BAKIZA), Dkt.Muhammed Seif Khatib (Mwenyekiti - BAKIZA), Dkt.Sewangi (Katibu Mtendaji- BAKITA) na Dkt.Samwel ( Mwenyekiti - BAKITA) na wajumbe wengine.