Thursday, September 10, 2015

MUHIMBLI YATOA MAFUNZO YA KUZUIA KIPINDUPINDU KWA WATUMISHI WAKE, 989 WAAMBUKIZWA.

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili –MNH-  imetoa  mafunzo kwa watumishi wake kudhibiti  ugonjwa wa kipindupindu   ambao  umesambaa na kusababisha watu 989 kuambukizwa  ugonjwa  huo  jijini Dar es salaam.

Mafunzo hayo ya siku saba ambayo yanahusisha Wakurugenzi, Wakuu wa Idara , Madaktari, Wauguzi , Wafamasia pamoja na Wahudumu  yana lengo la kuwaelimisha juu ya ugonjwa huo , jinsi ya kuzuia , kumtibu mgonjwa na kumtambua mtu mwenye dalili za Kipindupindu.

Akielezea  mafunzo hayo Mkuu wa Idara ya magonjwa ya dharura na ajali  ambaye  pia  ni Daktari Bingwa wa magonjwa  hayo  katika Hospitali ya Taifa Muhimbili  Dokta  JUMA   MFINANGA amesisitiza kuwa chanzo kikuu cha ugonjwa wa Kipindupindu ni uchafu lakini pia maji  machafu yanachangia kwa asilimia kubwa kuenea  kwa ugonjwa huo.

Hivyo amewakumbusha wananchi kuzingatia usafi  kwa kunawa mikono kwa sabuni  na maji yanayotiririka , kula vyakula vya moto , kunywa maji yaliyo safi na salama kusafisha  mazingira  na kwa wale wanaosafiri wametakiwa kutokula  hovyo barabarani kwani hali  bado ni tete.

Kwa mujibu wa Dokta MFINANGA  Hospitali ya Taifa  Muhimbili imepokea wagonjwa 20 ambao wanadalili za ugonjwa huo na kisha kupelekwa katika kambi za Kipindupindu.

Manispaa  ya  Kinondoni inaongoza kwakuwa na wagonjwa 663, Ilala ina wagonjwa 246 na Temeke ina wagonjwa 80.

            Mafunzo hayo yameanza leo yatamalizika Septemba 17 mwaka huu ambapo leo waaguzi 126  tayari wamepatiwa mafunzo hayo.

No comments:

Post a Comment