Thursday, September 10, 2015

BALOZI SEIF ALLI IDD: NIAIBU KUONA KIJIJI CHA MITAMBUUNI KUKOSE HUDUMA YA SKULI

 Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Wananchi na wana CCM wa Kijiji cha Mitambuuni alipofika kuwasailia akiwa katika ziara ya Kisiwa cha Pemba.
 Balozi Seif akisalimiana na Wanachama wa Chama cha Mapinduzi wa Kijiji cha Mitambuuni Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba, kulia yake ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba Mzee Mberwa Hamad Mberwa na kushoto yake ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM ya Mkoa huo Omar Khamis Othman.
 Baadhi ya Viongozi wa Chama cha Mapinduzi wakifuatilia hotuba ya Balozi Seif hayupo pichani wakati akizungumza na wana CCM na Vijana wa Maskani ya Vumilia ya Mitambuuni Wete Pemba.
Balozi Seif akiwapongeza Vijana wa Maskani ya CCM YA Vumilia ya Kijiji cha Mitambuuni baada ya kuamua kuuhama upinzani na kujiunga na Chama cha Mapinduzi.
Picha na –OMPR – ZNZ.

                                    
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba ni aibu kubwa kuona Wananchi wa Kijiji cha Mitambuuni  kiliopo Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba wanakosa  huduma za Skuli ya Maandalizi  kwa watoto wao wakati Wawakilishi na Wabunge wao wapo.

Alisema inasikitisha na kutia uchungu kutokana na kadhia inayowapata watoto wa Kijiji  hicho ya kufuata masomo umbali wa kilomita Sita matatizo ambayo yanaweza kupatiwa ufumbuzi  ndani ya uwezo wa Viongozi wao wa Jimbo.

Balozi Seif Ali Iddi alielezea masikitiko yake wakati  wa hafla fupi ya kuizindua Maskani ya CCM ya Vumilia ya Kijiji cha Mitambuuni Mkoa wa Kaskazini Pemba iliyoanzishwa na Vijana walioamua kuacha upinzani na kujiunga na Chama cha Mapinduzi .

Alisema Chama cha Mapinduzi katika kipindi kijacho mara baada ya uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba kinakusudia kufanya mabadiliko zaidi ya Maendeleo katika Majimbo la Kisiwa cha Pemba kwa lengo la kupunguza kero zinazowakabili Wananchi wa Majimbo hayo.

Balozi Seif aliwakumbusha na kuwaomba Wananchi wa Majimbo ya Kisiwa cha  Pemba  kuhakikisha kwamba wanawachagua Viongozi watakaokuwa tayari kufanya kazi nao.

Alisema wapo viongozi wengi wa Majimbo hayo wenye tabia ya kuyahama majimbo yao mara tuu bada ya kuchaguliwa na kuazisha Familia nyengine katika maeneo ya Unguja, Dar es salaam na Dodoma  na kusahau kwamba wamebeba dhima ya kuwatumikia wananchi waliowapa kura zao.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM aliwapongeza Vijana hao wa Kijiji cha Mitambuuni kwa uamuzi wao wa kufuata sera sahihi zinazotekelezeka za Chama tawala cha Mapinduzi.

Balozi Seif liwataka Vijana hao kwa kushirikiana na Wazazi na Viongozi wa eneo hilo kuanza maandalizi ya ujenzi wa  maskani yao ya kudumu pamoja na Skuli ya Maandalizi kwa hatua ya msingi
Aliwahakikishia wananchi na Vijana hao wa Mitambuuni kwamba atachukuwa juhudi za makusudi katika kuunga mkono uendelezaji wa  ujenzi wa majengo yote Mawili  ili  kusaidia kuwaondoshea changamoto zinazowakabili  watoto na Vijana hao.

Mapema Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Kaskazini Pemba Mzee Mberwa Hamad Mberwa  alisema Mtambwe na Vitongoji vyake imebadilika kutokana na Sera sahihi za Chama cha Mapinduzi zilizokuwa zikitekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mzee Mberwa alisema harakati za kiuchumi zimeongezeka  na kupanuka mara dufu  na kutoa fursa  pana zaidi kwa Wananchi  maeneo hayo kuendeleza vyema maisha yao  ya kila baada ya kukamilika kwa miundo mbinu bora ya mawasiliano ya bara bara.

Akisoma Risala ya Maskani hiyo ya CCM ya Vumilia  Mitambuuni  Katibu wa Maskani hiyo Ndugu Juma Said Saleh alisema uamuzi wa vijana hao kuuhama upinzani  na kuhamia CCM unatokana na  tabia ya viongozi wanaowachaguwa kutokujali kuwatumikia.

Nd. Said alisema dharau ZA Viongozi hao zimesababisha kuibuka kwa changamoto kadhaa zisizopaswa kutatuliwa na Serikali Kuu ambazo zimo ndani ya uwezo  kamili wa Viongozi wao wa Majimbo.

Katibu huyo wa Maskani ya Vumilia alieleza kwamba Vijana hao katika kupambana na tabia ya Viongozi hao wameahidi kufanya kampeni ya nyumba hadi nyumba katika kuhakikisha  Wagombea Uchaguzi kupitia Chama cha Mapinduzi wanaibuka washindi ili waweze kuwatumikia kwa upendo na ushirikiano.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
9/9/2015.

No comments:

Post a Comment