Wednesday, October 14, 2015

TANO ZA MAGUFULI . UADILIFU .UCHAPAKAZI .UFUATILIAJI .UTEKELEZAJI NA UTUMISHI ULIOTUKUKA

MGOMBEA urais wa CCM, Dk John Magufuli amewataka wananchi kumchagua ili awe rais wa tano ajaye wa Tanzania huku akiahidi kushughulikia masuala mbalimbali ya wananchi na hivyo kuliletea Taifa maendeleo kwa muda wote atakaokuwepo madarakani.

Akizungumza na wananchi wa mkoani Lindi katika muendelezo wa kampeni zake, Dk Magufuli alisema akichaguliwa kushika nafasi hiyo, pamoja na mambo mengine atakayoyafanya atatumia utajiri wa gesi uliopo katika mikoa ya Kusini, kutoa ruzuku kwa vifaa vya ujenzi ili kushusha bei na kuwawezesha wananchi kujenga nyumba bora.

Amesema pia atatumia nafasi hiyo kutafuta namna bora ya kuwainua wakulima wa korosho, tofauti na utaratibu wa sasa wa stakabadhi ghalani, alisema umekuwa ukiwasababishia umasikini mkubwa wakulima wa zao hilo.
Akiwa Nachingwea, Ruangwa, Mtama na Lindi Mjini, Dk. Magufuli alisema tofauti na wapinzani wanaoahidi kuondoa nyumba za nyasi na tembe nchi nzima kwa siku 100 watakazokaa Ikulu, jambo alilosema ni ndoto, Serikali yake itakachofanya ni kushusha bei ya mabati, saruji, nondo, misumali na vifaa vingine vya ujenzi ili wananchi wajenge nyumba bora.

Akielezea ni vipi atawezesha hilo kufanikiwa, Dk Magufuli alisema atatumia utajiri wa rasilimali za Taifa ikiwemo gesi inayopatikanakatika Mikoa ya Kusini na Bagamoyo, Pwani ili kutoa ruzuku katika vifaa vya ujenzi.

Lakini, pia kuongeza viwanda vya bidhaa hizo ili kushusha bei kwa kiwango cha juu. Alisema dalili za kushuka kwa vifaa hivyo, zimeanza kuonekana baada ya kujengwa kwa Kiwanda cha Saruji cha Dangote mkoani Mtwara, ambachokinatumia nishati ya gesi kwa uzalishaji, kilichowezesha kushuka kwa bei ya saruji kutoka Sh 16,000 hadi Sh 8,000 na kwamba bei hiyo itashuka zaidi atakapokuwa rais.

Alisema pia ataziba mianya yote ya rushwa serikalini ili makusanyo ya fedha hizo yatumike kuboresha maisha ya Watanzania wakiwemo wa Kusini, huku akisema ushahidi wa utendaji wake kwa watu wa Kusini ni ujenzi wa barabara za lami kutoka Dar es Salaam kwenda Lindi na Mtwara na baadaye Tunduru na Songea.

Ili kumwezesha kuingia Ikulu, mgombea huyo aliwaomba wakaziwa Mkoa wa Lindi kufika katika vituo vya kupiga kura mapema asubuhi ya Oktoba25, huku akisema kutokana na vitisho na vurugu zilizopangwa ili kuwatishia wananchi hasa wanawake wasipige kura, kutakuwa na polisi wa kutosha ili kulinda amani.

Akizungumzia soko la korosho, Dk Magufuli alisema akiingiaIkulu atabadili mfumo wa ununuzi wa korosho ili kuwezesha wakulima wa zao hilo kwa mikoa ya Kusini, kunufaika na kuboresha maisha yao na kuachana na mfumo wasasa ambao unawafanya wakulima kukopwa fedha zao bila kulipwa na hivyo kuwa masikini.

No comments:

Post a Comment