Mwenyekiti wa Mtandao wa Kimataifa wa Wabunge (PGA) Mhe. Pindi Chana ( MB) akimkabidhi Rais wa Baraza Kuu la 70 la Umoja wa Mataifa, Bw.Mogens Lykketoft,Tamko la wabunge lenye sahihi 607 za wabunge kutoka mataifa 70 la kutokomeza ndo za utotoni na za kulazimisha katika hafla fupi iliyofanyika Umoja wa Mataifa siku ya Jumatatu.
Mwakilishi wa Kudumu wa Zambia katika Umoja wa Mataifa, Balozi Dr. Mwaba Kasese-Bota akizungumza wakati wa hafla hiyo ambapo alianisha mipango mbalimbali inayofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwamo viongozi wa kimila katika kuzunguia ndoa za utotoni na za kulazimishwa.
Mwakilishi wa Kudumu wa Ghana katika Umoja wa Mataifa, Balozi Martha Anna Akyaa Pobea naye akitoa mchango wa namna gani serikali yake inavyolishughulikiwa tatizo za ndoa za utotoni ambapo amesema katika nchi za Afrika Magharibi katika kila watoto watano wa kike, wawili huolewa kabla ya kutimiza miaka 18 na kwamba ndoa hizo za utotoni si tu kwamba zinadumaza ukuaji wake lakini pia zinachaniga mimba za umri mdogo, vifo vitokanavyo na uzazi, maambukizi ya magonjwa mbalimbali na kuchangia umaskini kwa watoto wengi wa kike.
Sehemu ya washiriki wa hafla hiyo wakiwamo watalamu kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto wakiongozwa na Kaimu Katibu Mkuu, Bi, Nuru Milao.
Na Mwandishi Maalum, New York
Mtandao wa Kimataifa wa Wabunge kutoka Mabunge mbalimbali Duniani (PGA), umemkabidhi Rais wa Baraza Kuu la 70 la Umoja wa Mataifa Bw. Mogens Lykketoft, tamko la kukomesha ndoa za utotoni na za kulazimishwa kwa watoto wa kike.
Akikabidhi tamko hilo lenye sahini Zaidi ya 607 kutoka nchi 70 Mwenyekiti wa Mtandao huo wa wabunge, Mhe. Pindi Chana na ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto amesema, kukabidhiwa kwa tamko hilo kwa Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kunakwenda sambamba na maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike ambayo huadhamishwa kila Octoba ya mwaka.
Mwenyekiti wa PGA, amesema wakati wa hafla hiyo fupi iliyofanyika hapa Umoja wa Mataifa, siku ya Jumatatu kwamba, ushirikiano wa wadau mbalimbali hasa wabunge , serikali na asasi za kiraia ni muhimu sana ikiwa jumuiya ya kimataifa inataka kuondokana na kumaliza tatizo la ndoa za utotoni na za kulazimishwa.
Mhe. Pindi Chana, amesema, ni kwa kutambua ukweli huo ndiko kulikopelekea kuanzishwa kwa mtandao huo mwezi Machi mwaka huu ambao moja na dhumuni lake kubwa ni kuwahamasisha, kuwaelimisha na kuwawezesha wabunge kutumia nafasi zao kukemea tatizo hilo.
Hafla hiyo iliandaliwa kwa ubia kati ya Wakilishi za Kudumu za Tanzania, Zambia , Ghana na Canada katika Umoja wa Mataifa. nchi ambazo kwa namna moona ama nyingine zimekuwa mstari wa mbele katika kuchangiza afya na maendeleo ya mtoto wa kike ili mtoto huyo wa kike aweze kupata fursa kukua, kuelimika na hatimaye aweze kulitumikia taifa lake na watu wake katika ukamilifu wake.
Amebainisha kwamba kama viongozi, wabunge wanapashwa kuwahabarisha wananchi wao, na wabunge wenzo thamani ya mtoto wa kike, na umuhimu wa kuhakikisha kuwa mtoto wa kike anakwenda shule, anabaki shule na anamaliza masomo yake.
“ Kama watunga sheria, wabunge tunapaswa kusimamia sheria zinazomlida mtoto wa kike ikiwa ni pamoja na kupitisha sheria zitakazo ainisha bayana umri wa kuolewa kwa mtoto wa kike ambao unapashwa kuwa miaka kumi na nane” amesititiza Mwenyekiti wa PGA.
Aidha Mhe.Pinda Chana akaongeza pia kuwa wabunge na mabunge yanao wajibu wa kusimamia utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu, na ugawaji wa raslimali kwenye maeneo mpaya ya kisera na sera ambazo tayari zipo.
Akaongeza kuwa Lengo namba 5.3 la maendeleo endelevu linaainisha wazi wazi namna ya kushughulikia vitendo vinavyorudisha nyuma maendeleo na ustawi wa mtoto wa kike katika kile eneo, jambo analosema wabunge wanapashwa kusimamia vema utekelezi wa lengo hilo pamoja na mengine.
PAG inalenga pia kuwaelimisha wabunge kutetea na kusimamia haki zinazomlinda mtoto wa kike, kupiga vita mila na desturi potofu zinazomkandamizi mtoto wa kike , kusimamia utawala wa sheria, demokrasia usawa wa binadamu, kupinga ubaguzi na kusimamia usawa wa kijinsia.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa tamko hilo, Rais wa Baraza Kuu la 70 la Umoja wa Mataifa, Bw. Lykketoft amesema kuwa tamko hilo limekuja wakati muafaka na hasa baada ya Viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali kupitisha kwa kauli moja Malengo Mapya ya Maendeleo Endelevu ( Agenda2030) mwezi uliopita.
Akaongeza kuwa, akiwa Rais wa Baraza Kuu la 70 atahakikisha kwamba nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zinaendelea na majadiliano yenye tija na yakayolenga katika kuhakikisha utekelezaji wa Agenda 2030 na kutilia mkazo mijadala inayolenga katika mkomboa mtoto wa kike dhidi ya ndoa za utotoni na za kulazimishwa. Na pia kuhakisha kwamba majadiliano kuhusu mabadiliko ya tabia nchi yanafanyika kwa lengo la siyo tu kuiokoa sayari dunia lakini pia maisha ya mwanadamu ambayo uhai wake unategemea sana uwepo wa sayari hiyo.
No comments:
Post a Comment