Mke wa Rais na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi,CCM, Mama Salma Kikwete akimnadi mgombea Urais kupitia CCM, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika uwanja wa Mpilipili huko Lindi Mjini tarehe 12.10.2015.
Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi Dkt. John Pombe Magufuli akimpongeza Mke wa Rais na Mjumbe wa NEC, Mama Salma Kikwete mara baada ya kumwombea kura kwa wananchi wa Manispaa ya Lindi kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa Mpilipili tarehe 12.10.2015. Aliyesimama kulia ni Mgombea Ubunge katika Jimbo la Mtama Ndugu Nape Nnauye.
Mke wa Rais na Mjumbe wa NEC Mama Salma Kikwete akiwa katika kijiji cha Ngunichile kilichoko katika Wilaya ya Nachingwea kwa ajili ya kuwanadi wagombea wa Chama Cha Mapinduzi kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika tarehe nchini tarehe 25.10.2015. Katika mikutano hiyo Mama Salma alimnadi Dkt. John Magufuli kwenye urais na Ndugu Hassan Elias Masala kwenye Ubunge wa Jimbo la Nachingwea na Madiwani wote katika wilaya hiyo tarehe 13.10.2015.
Na Anna Nkinda – Maelezo, Liwale
Na Anna Nkinda – Maelezo, Liwale
Wananchi wa mkoa wa Lindi wameaswa kufanya kazi kwa bidii ili waweze kujiletea mabadiliko ya kweli katika maisha yao kwani kuna baadhi ya watu hawapendi kufanya kazi huku wakisubiri mabadiliko.
Rai hiyo imetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea kwa nyakati tofauti na wananchi wa vijiji vya Ngunichile na Mbaya vilivyopo katika majimbo ya Nachingwea na Liwale waliohudhuria mkutano wa kampeni ya kuwanadi wagombea wa nafasi za udiwani, ubunge na urais kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mama Kikwete ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kupitia wilaya ya Lindi mjini alisema mabadiliko ya kweli hayawezi kupatikana bila ya kufanya kazi kwani kuna baadhi ya watu hasa vijana hawafanyi kazi wakiamka asubuhi kitu wanachokifanya ni kucheza pool huku wakisubiri mabadiliko.
“Hata katika vitabu vya dini imeandikwa asiyefanya kazi na asile kwani kazi ni msingi wa maendeleo, hata ukipiga kelele kiasi gani kama hufanyi kazi huwezi kupata mabadiliko katika maisha yako”.
“Ndugu zangu Mwenyezi Mungu ametupa akili ya kutambua mema na mabaya tusikubali kudanganywa, mabadiliko ya siku hizi siyo mazuri yanaleta uvunjifu wa Amani kwani watu wamepandikizwa maneno ya chuki wanafanya vurumai na kuharibu vya kwao, wanawachukia ndugu zao imefikia hatua watu hawazikani, hawasalimiani. Lakini hao aliowapandikiza chuki kwao kuna maendeleo”, alisisitiza.
Mama Kikwete alisema yeye kama MNEC anadhamana kubwa ya kuhakikisha anakisemea na kukipigania chama chake na kuwataka wananchi hao kushikamana na kuwa kitu kimoja kwa kufanya hivyo wataitunza Amani ya nchi na kuzidi kudumisha upendo katika jamii yao.
Aidha aliwasihi wananchi hao kutokubali kurubuniwa na kitu chochote bali wazitunze kadi zao za kupigia kura na siku ya uchaguzi ikifika wasipoteze haki yao ya msingi ya kupiga kura wajitokeze kwa wingi na kuwachagua viongozi kutoka CCM ambao watawaletea maendeleo ya kweli.
Kwa upande wake mgombea ubunge jimbo la Nachingwea Hassan Massala aliahidi kama atachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo atasimamia ilani ya uchaguzi ya CCM na kuhakikisha huduma za elimu zinaboreshwa hii ni pamoja na shule kuwa na vitabu na walimu wa kutosha na kujenga nyumba za walimu ili watoto wapate elimu bora. Ataboresha huduma za afya ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na Zahanati na dawa zinapatikana kwa wakati.
Massala alisema, “Katika jimbo hili, maeneo ya mjini kuna maji ya kutosha lakini kijiji cha Ngunichile kuna tatizo ingawa vyanzo vya maji vipo. Nitahakikisha maji yanapatikana. Kuhusu umeme Serikali inampango wa kusambaza katika vijiji vyote, nguzo zimeanza kusambazwa kinachohitajika ni kusimamia ili zoezi hili liende haraka”.
Mgombea huyo wa nafasi ya Ubunge alimuomba Mama Kikwete awasaidie ili mnara wa mawasiliano ya simu uweze kujengwa katika kata ya Ngunichile kwani eneo hilo linashida ya mawasiliano.
“Ukiwa katika kijiji hiki huwezi kuwasiliana na mtu yeyote kwa njia ya simu kwa kuwa hakuna mnara wa mawasiliano. Hivi sasa simu ni pesa na simu ni Benki tunaomba Mama yetu utusaidie ili mnara wa mawasiliano ujengwe katika kijiji hiki”, Massala aliomba.
Kuhusu ombi la kujengewa mnara wa mawasiliano ya simu katika kijiji hicho ambacho ni kata ya Ngunichile Mama Kikwete aliahidi kulifanyia kazi na kulifikisha kunakohusika.
Naye mgombea ubunge wa jimbo la Liwale Faith Mitambo aliwaomba wananchi wamchague ili aendelee kuwatumikia kwa kipindi kingine cha miaka mitano na kuhakikisha maendeleo yanazidi kupatikana katika jimbo hilo.
Mitambo alisema, “Ilani ya uchaguzi ya CCM inasema itaendelea kuboresha huduma ya afya na ndani ya mwaka mmoja baada ya uchaguzi Zahanati ya kijiji cha Mbaya itakuwa kituo cha Afya. Aidha Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni tatu kwa ajili ya kuhakikisha umeme unapatikana vijijini kati ya vijiji hivyo kimojawapo ni kijiji hiki.
“Nawaomba kura zenu ili mtuchague viongozi kutoka CCM ambao ni madiwani, mbunge na rais ili tuweze kusimamia na kutekeleza kwa vitendo na kuhakikisha yale yote yaliyoandikwa katika ilani ya uchaguzi yanatekelezwa”,.
No comments:
Post a Comment