Sunday, October 18, 2015

MAALIM SEIF BUBUBU

MGOMBEA Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, ameahidi kuweka mazingira bora kwa wafanyabiashara wakubwa na wadogo iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu ujao.

Akiwahutubia wafuasi wa Chama hicho katika mkutano wa kampeni uliofanyika viwanja vya Kwageji Bububu, Maalim Seif amesema atarekebisha mfumo wa ushuru katika bandari ili kuepusha wafanyabiashara kulipa ushuru mara mbili wanaposafirisha mizigo yao kuelekea bandari ya Dar es Salaam.

Amesema hali hiyo imekuwa ikiwadhoofisha wafanyabiashara wa Zanzibar, jambo amesema ataliwekea utaratibu mzuri, ili wafanyabiashara waweze kuendesha shughuli zao bila ya usumbufu.

Akizungumzia wafanyabiashara wadogo wadogo wakiwemo wale wa Jua kali, Maalim Seif amesema atawaekea mazingira mazuri kuweza kufanya shuguli zao.

Amesema chini ya uongozi wake iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar atahakikisha kuwa wafanyabiashara hao hawanyanyaswi, na watawekewa maeneo maalum ya kufanya biashara zao, na kwamba hakutokuwa na ulipaji wa kodi zisizotambulika katika maeneo yao.

Aidha ameahidi kuanzisha benki ya uwekezaji, ili kukuza mitaji ya wafanyabiashara wadogo wadogo.

Nae afisa uchaguzi wa CUF Bw. Muhene Said Rashid, amewataka wanachama hao kuweka utaratibu mzuri wa kuwasaidia wasioweza kupiga kura wakiwemo wagonjwa, wazee na wenye ulemavu,  ili kila aliyejiandikisha aweze kupiga kura kwa mgombea anayemtaka.

Aidha amewataka kuelimishana juu ya namna ya upigaji kura, ili kuepuka uharibifu wa kura na kupiga kura kwa usahihi.

 Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiwahutubia wafuasi wa Chama hicho katika viwanja vya Kwageji Bububu.

  Wafuasi wa CUF wakisikiliza na kushangilia hotuba ya mgombea Urais wa Chama hicho katika viwanja vya Kwageji Bububu.
 Imail Jussa Ladhu, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Timu ya Ushindi CUF, akihutubia kwenye mkutano huo. (Picha na Salmin Said, OMKR)

No comments:

Post a Comment