Na Swahilivilla Blog Washington
Waziri Majivuno wa Kusadikika alisema: "Hekima ni kitu adimu kupatikana kwa mtu asiye na mvi...". Pia Waswahili wanasema: "Akili ni nywele"
Mshitakiwa Karama aliipinga hoja ya Waziri Majivuno kwa kusema: "....Elimu ilipokuwa haijulikani hapa duniani, mvi zilizingatiwa kuwa ni ishara ya hekima..."
Nimekuwa nikiyatafakari mafungu hayo matatu ya maneno ili kuona kama yana uhalisia wowote katika maisha yetu ya leo.
Pichani Ndugu Saidi Mwamende akimuliza swali Mhe: Jussa, (Hayupo Pichani)
Hivi majuzi swahibu yangu Said Mwamende alinipigia simu na mara tu baada ya kuijbu, nilihisi sauti yake imejaa furaha, ndipo nikamwuliza ''umepandishwa cheo?"
Akanijibu: "Hapana, bali nimekuwa nikifuatilia siasa za Tanzania zinavyokwenda na nikakumbuka ule mkutano wa Mheshimiwa Ismail Jussa alioufanya na Wanadiaspora hapa Washington. Yale aliyoyasema ndiyo yanayoendelea kutokea hivi sasa".
Nikakurupuka kuchakura maktaba yangu kuitafuta rekodi ya mkutano ule ili nijikumbushe aliyoyasema Mheshimiwa Jussa.
Baada ya kuiangalia tena, nikaona sehemu ambayo Swahibu yangu Said Mwamende alimwuliza Mheshimiwa Jussa swali ambalo lilihitaji mwono na mtazamo wa kina wa kisiasa:
"Je, UKAWA, tuseme, kwa upande wa chama chako wewe atakuwepo Mheshimiwa Lipumba, na tuseme kwa upande wa CHADEMA Mzee wetu Mbowe. Watu hawa tayari wameshagombea Urais. Je hamuoni kwa CCM kwa sasa hivi kuna hombwe la aina fulani? Kuna Mheshimiwa Lowassa inawezekana kwamba hatogombea CCM kutokana na labda hawatomtaka. Mnafikiriaje UKAWA kama mtamchukua yule Lowassa ili mumuweke pale agombee?"
Kwa ulimi wa fasaha kuliko wa Karama wa Kusadikika, Mheshimiwa Jussa alilijibu swali la Bwana Mwamende ambaye ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Watanzania katika Jiji la Washington na Vitongoji vyake (DMV), kwa kusema:
"Katika siasa, wiki moja inaweza kuwa muda mrefu sana". Aliendelea kwa kusema kuwa siyo Lowassa tu, anaweza kupitishwa Loawassa akaachwa mtu mwengine mwenye ugomvi na Lowassa vilele. Kwa sababu CCM hivi sasa siyo chama tena kinachowaunganishwa na itikadi. Kinachowaunganisha ni Escrow na kwamba kila mmoja atapata mgao wake kiasi gani".
Mhe: Ismail Jussa akijibu swali la Saidi Mwamende (Hayupo pichani)
Katika mkutano huo uliofanyika tarehe 28 Februari mwaka huu jijjini Washington, Bwana Ismail Jussa, aliwathibitishia Wanadiaspora wa Tanzania nchini Marekani pamoja na ulimwengu kwa ujumla kuwa Elimu ilipokuwa haijulikani hapa duniani, mvi zilizingatiwa kuwa ni ishara ya hekima, lakini nadharia hiyo wakati wake umepita na hautorejea tena.
Kwani katika kujibu swali la Katibu wa Jumuiya ya Watanzania kwaishio jijini Washington na vitongoji vyake Bwana Said Mwamende, Mheshimiwa Jussa alisema ni mapema mno kulitolea kauli swala hilo, ispokuwa "nitasema moja ambalo litatosheleza swali lako"
'Moja' hilo la Mwakilishi huyo wa Jimbo la Mji Mkongwe, Zanzibar ambaye nywele zake bado ni nyeusi, linathibitisha kuwa nafasi hiyo aliyonayo kupitia ridhaa ya wananchi wa Jimbo lake hakuipata kwa sudfa tu, bali alistahiki na anaistahiki. Bali ni Mwanasiasa aliyekomaa na mwenye kuona mbali.
"Nilisema mapema kwamba nazungumza na Mwenyekiti Mbowe, nazungumza na Mwenyekiti Lipumba na nazungumza na Mwenyekiti Mbatia. Sioni kwamba kwa wote hao kuna fikra ya ung'ang'anizi kwamba lazima niwe mimi". Alisema Bwana Jussa kwa kujiamni, na kusisitiza "Hilo silioni kwa sasa hivi".
Upana wa wigo wa mawasiliano yake hayo unadhihirisha ukomavu wa akili yake, na kwamba fikra zake hazikufungika ndani ya vichochoro vya Mji Mkongwe, bali zimevuka Bahari ya Hindi na kuangaza Tanzania yote na hata nje ya mipaka yake.
Mheshimiwa Jussa hakuwa anastawisha Baraza tu au 'kumwondosha njiani' Bwana Mwamende, bali alikuwa anazungumzia uhalisia wa mambo yanavyopaswa kuwa. Aidha hakuwa akitumia ulaghai wa kisiasa pale aliposema: "Na ninachojua ni kwamba viongozi wetu wanaangalia hata nje ya vyama katika kupata mgombea ambaye ataweza kuwakilisha vyema misimamo na ajenda ambayo UKAWA inaisimamia".
Bwana Jussa ambaye kitaaluma ni msoni wa Sheria, alidhihirisha wazi kipaji chake cha kuweza kushtukia na kufichua mbinu sa kisiasa zilizojificha. Aidha si mtu anayekhofu kuelezea maoni yake binafsi kwa manufaa ya umma. Haya yanaonekana alipoendelea kunena:
"Nikwambie kitu kimoja, hili ni mawazo yangu binafsi: 'Mimi nahisi CCM wana khofu na hilo unalolisema kama Chama. Na ndiyo maana tulikuwa tunajua sote kwamba CCM ilikwisha tangaza kwamba Mkutano wao Mkuu wa kumpata mgombea ulikuwa umepangwa kufanyika mwezi wa April. Lakini juzi tulimsikia Nape Nnauye akisema kuwa kutokana na sababu ya kura ya maoni, na Bunge la Bajeti linofuata baadaye, itakuwa vinaingiliana. Kwa hivyo bora uakhirishwe mpaka baada ya Bunge la Bajeti'.."
Kigogo huyo wa Chama Cha Wananchi CUF, aliitafsiri kauli hiyo ya CCM kama ni mbinu ya kuvuta wakati na kwenda karibu na uchaguzi wakidhani wataweza kuliepuka jambo hilo.
"Kwa hiyo, tafsiri yangu ni kwamba wanataka kwenda zaidi, ili wakidhani wataweza kuliepusha hilo" Alichambua bwana Jussa ambaye kadiri nywele zake zinavyopotea, ndivyo akili zake zinavyozidi kukomaa.
Pichani Makamu Mwenyekiti wa CUF wakati huo, Maalim Seif Sharif Hamad (kulia) na Mwakilishi wa sasa wa Mji Mkongwe, Ismail Jussa.
Tangu ujanani mwake, Mheshimiwa Ismail Jussa alikuwa akipenda kukaa na watu wazima akijua kuwa huko ndiko kwenye hazina za hekima na maarifa. Mwenendo wake huo, ndio uliopanua muono wake na kuweza kuichambua CCM na kuielezea kuwa ni Chama kilichopoteza mwelekeo, itikadi na misingi kiliyoasisiwa chini yake, na kwamba kilichobaki ni makundi makundi ndani yake yenye kupigania maslahi binafsi.
"Kwa jinsi ninavyoona, ile CCM ya Nyerere ambayo mpo pale kwa sababu ya Ujamaa na Azimio la Arusha haipo tena. Kilichobakia ni kwamba ni vipi kila mtu na kundi lake na rafiki zake watafanikiwa kupata nafasi wakavuruge nchi"
Jussa si mtu wa papara wala pupa, bali mtu ni mwenye subira, na alimtaka Bwana Mwamende kujiunga naye katika mbuga ya subira na kuupa nafasi wakati ufanye kazi yake.
"Kwa hiyo ninachosema, hayo tuyaachie wakati wake ukifika. Kama atatoka miongoni mwa hao, kama atatoka nje ya hao, au kama atatoka miongoni mwa viongozi wa UKAWA tuuachie wakati utasema".
Aidha kwa mara nyengine alisisitza imani yake juu ya viongozi wa Vyama vinavyounda UKAWA juu ya msimamo wao wa kuwa na mgombea mmoja:
Nataka nikuhakikishie kuwa kwa upande wa UKAWA si hoja kwamba awe Lipumba, Slaa, Mbowe au Mbatia. Si hoja kabisa kwa sasa hivi. Hoja ni nani ataweza kubeba bendera ya UKAWA"
Mheshimiwa Jussa alimalizia jibu lake kwa kusema "Nadhani tutafika vizuri".
Kauli hiyo ilikuwa inatabiria "Safari ya Matumaini" ya Mheshimiwa Edward Lowassa iliyogeuka na kuwa "Safari ya Uhakika".
Naam, akili si nywele, na wala mvi si dalili ya hekima. Bali elimu ndiyo mwangaza, khaswa pale inapotiliwa nguvu na tabia ya kukaa na watu wenye busara. Maneno aliyoyasema Mheshimiwa Jussa tarehe 28 Februari 2015 nchini Marekani, ndiyo ambayo leo hii yanatuongozea siasa za Tanzania.
No comments:
Post a Comment