Friday, October 16, 2015

MKOA WA MJINI MAGHARIBI

Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiwahutubia wafuasi wa Chama hicho katika viwanja vya Fumba Kids, jimbo la Dimani. 
 Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akimtambulisha mgombea Uwakilishi wa jimbo la Dimani kupitia chama hicho Bw. Mohamed Hashim Ismail, katika mkutano uliofanyika viwanja vya Fumba Kids.
 Wafuasi wa CUF wakifuatilia hotuba na mgombea urais wa Chama hicho katika viwanja vya Fumba Kids, jimbo la Dimani.
 Afisa uchaguzi wa CUF Bw. Muhene Said Rashid, akitoa elimu ya wapiga kura kwa wafuasi wa chama hicho kwenye mkutano uliofanyika viwanja vya Fumba Kids, jimbo la Dimani.
Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiungana na wafuasi wa CUF kuimba nyimbo za kuhamasisha alipowasili katika barza ya “Radio One” kuonana na wanabarza hiyo. (Picha na Salmin Said, OMKR)
 
MKOA WA MJINI MAGHARIBI          
Na: Hassan Hamad, OMKR
Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amesema iwapo atachaguliwa kura Rais atazipitia upya fidia walizolipwa wananchi wa maeneo ya Fumba, Bwefumu na Bweleo ili kuwalipa fidia zinazostahiki kulingana na maeneo yao yaliyochukuliwa kwa ajili na uendelezaji wa maeneo huru ya kiuchumi.

Amesema serikali atakayoiongoza iwapo atachaguliwa kuwa Rais inakusudia kuondosha kabisa vitendo vya dhulma dhidi ya wananchi, hivyo wananchi hao watapatiwa fidia zinazostahiki baada ya kufanyiwa tathmini.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni za chama hicho uliofanyika viwanja vya Fumba jimbo la Dimani, Maalim Seif amesema Serikali inapaswa kulipa fidia zinazoendana na thamani ya maeneo ya wananchi inapoamua kuyachukua kwa maslahi ya umma, na kwamba serikali yake haitosita kufanya hivyo katika maeneo ya ukanda wa Fumba.

Aidha Maalim Seif amewahakikishia wananchi wa maeneo hayo upatikanaji wa maji safi na salama, ili kuondosha kabisa tatizo hilo linalowakabili kwa muda mrefu sasa.

Akizungumzia kuhusu mchakato wa uchaguzi Maalim Seif amesema licha na vitendo vinavyofanywa kuashiria kuingilia kati mchakato huo, uchaguzi mkuu utafanyika tarehe 25 Oktoba kama ulivyopangwa.

Kabla ya mkutano huo Maalim Seif alifanya ziara ya kutembelea baadhi ya matawi na barza za majimbo ya Kijitoupele, Dimani Mwanakwerekwe na Welezo ikiwemo barza ya “Radio One” na kuelezea kuridhishwa na jinsi wananchi walivyohamasika kushiriki  uchaguzi ujao.
 
Nae Mgombea Uwakilishi wa jimbo la Dimani kupitia chama hicho Bw. Mohamed Hashim Ismail amewataka wananchi wanaoitakia mema Zanzibar kuwachagua wagombea waliosimamisha na Chama Cha Wananchi CUF katika uchaguzi ujao ambao amesema ni muhimu kwa ukombozi wa Zanzibar.

Amesema akiwa mgombea wa jimbo hilo atahakikisha kuwa anapita nyumba kwa nyumba ili kuona kuwa kila aliyejiandikisha kupiga kura wakiwemo wagonjwa wanatekeleza jukumu hilo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Timu ya ushindi CUF Mhe. Ismail Jussa Ladhu  amelishauri jeshi la polisi kuendeleza mahumiano mema kati yake na wananchi kama lilivyofanya wakati wa kuanza kwa kampeni.

Amesema  ni vyema kwa jeshi hilo kufanya juhudi za kudhibiti vitendo vinavyoashiria shari ikiwa ni pamoja na baadhi ya hujuma vinazofanywa dhidi ya majengo na wanachama wa chama hicho.

No comments:

Post a Comment