Na Lucas Mboje, Dar es Saam
KAIMU Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Dkt. Juma Malewa (pichani)
amewaasa Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza nchini kuzingatia kuwa
utendaji wao wa kazi za kila siku uende sambamba na kasi ya Serikali ya Awamu
ya tano ili kuleta ufanisi unaotarajiwa.
KAIMU Kamishna Jenerali, Dkt. Malewa ameyasema hayo jana wakati wa Baraza la
Kufunga Mwaka 2016 na kuukaribisha Mwaka 2017 lililowahusisha baadhi ya Maafisa
na Askari kutoka Ofisi ya Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, Chuo cha Taaluma ya
Urekebishaji Ukonga, Kikosi Maalum cha Kutuliza Ghasia Magerezani pamoja na
Magereza ya Mkoa wa D'Salaam.
Aidha, amewataka Maofisa na Askari wa Jeshi hilo kudumisha nidhamu wanapokuwa
wakitekeleza majukumu yao ya kazi
ikiwemo kutekeleza mara moja Amri mbalimbali zinazotolewa na Viongozi wao
wa Jeshi.
"Kila mmoja wenu atimize wajibu wake katika eneo lake la kazi kwa bidii,
ari na moyo wa kujituma ili kuliwezesha Jeshi letu kupata ufanisi unaotarajiwa".
Alisisitiza Kaimu Jenerali Dkt. Malewa.
Wakati huo huo Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Dkt. Juma Malewa pia ametumia fursa hiyo kuelezea baadhi ya
mafanikio mbalimbali yaliyopatikana kwa Mwaka uliopita 2016 ambapo Jeshi la
Magereza limeweza kupata jumla ya leseni 102 za uchimbaji wa madini ya ujenzi
kama vile chokaa, mawe, kokoto, mchanga na Murram katika maeneo mbalimbali ya
magereza. Pia katika mwaka 2016 Jeshi limeweza kujenga nyumba 129 kwa njia ya
kujitolea ambapo nyumba 231 zipo katika hatua mbalimbali ya ukamilishaji.
Aidha, Ujenzi wa nyumba 320 za
makazi ya askari katika eneo la Gereza Ukonga maandalizi ya ujenzi yanaendelea na
ujenzi wa nyumba hizo ni kufuatia ziara ya Rais Magufuli Novemba 29 mwaka huu ambapo alipokea taarifa ya uhaba wa nyumba za
kuishi askari wa jeshi hilo na akaagiza Jeshi la Magereza lipatiwe Tsh. bilioni
10 haraka ili kupunguza tatizo hilo.
Shirika la Magereza na Mfuko wa hifadhi ya Jamii wa PPF wameingia Makubaliano
ya Mkataba wa ubia katika mradi wa ujenzi wa Kiwanda kipya cha kusakata ngozi
pamoja na uwekezaji wa mashine za kisasa za kutengnezea bidhaa za ngozi katika
Kiwanda cha Viatu cha Gereza Karanga, Moshi.
Chuo cha Maafisa Magereza Ukonga kimepata
Ithibati na hivyo kuwa na hadhi ya kuwa Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji na mapema mwakani
kinatarajia kudahili wanafunzi 30 katika fani ya Taaluma ya Urekebishaji ngazi
ya cheti.
Pamoja na Mafanikio hayo, Kaimu Kamishna Jenerali Dkt. Malewa ameelezea
changamoto mbalimbali zinazolikabili Jeshi hilo ikiwemo ufinyu wa bajeti,
makazi duni ya maofisa na askari, uhaba wa vitendea kazi, ukosefu wa pembejeo pamoja
na madeni ya wabuni na watumishi wa jeshi hilo.
Kuhusu maeneo yatakayopewa kipaumbele
kwa Mwaka mpya 2017 ni kuwa Jeshi la Magereza litaendeleza jitihada za
kuimarisha na kuongeza uzalishaji kwenye miradi ya uzalishaji wa mazao ya
Kilimo na mifugo lengo ikiwa ni kujitosheleza kwenye chakula cha wafungwa,
kuhakikisha wafungwa wanafanya kazi za uzalishaji mali kwa kiwango chenye tija
badala ya kukaa tu magerezani pia kuendeleza mikakati ya kupunguza msongamano
magerezani.
Baraza la kufunga Mwaka na kuukaribisha Mwaka unaofuata ni utamaduni wa siku
nyingi ambao unaenziwa na Viongozi Wakuu wa Jeshi la Magereza ambapo Baraza la
aina hii hufanyika kila Mwaka ili Kamishna Jenerali wa Magereza nchini aweze
kuongea na Watumishi wote wa Jeshi la Magereza nchini kupitia Baraza hilo lengo
ikiwa ni kufanya tathmini ya yale yaliyojiri katika Jeshi kwa kipindi cha Mwaka
unaisha kwa kuzungumzia mafanikio na changamoto zilizojitokeza na
kutazama matarajio ya Mwaka mpya.